Kwa Umoja wa Mataifa(ONU), “ulinzi wa raia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (RDC) unabaki kuwa kipaumbele muhimu,” kulingana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Idara ya Ulinzi wa Amani, Jean-Pierre Lacroix.
Alithibitisha haya Jumatatu, tarehe 16 Septemba, mjini Kinshasa, baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa RDC, Thérèse Wamba Wagner.
Akizungumza na waandishi wa habari, Jean-Pierre Lacroix alizungumzia suala la ulinzi wa raia kutokana na hali ya kibinadamu inayotokea mashariki mwa nchi. Kwa maoni yake, ulinzi wa raia unabaki kuwa kipaumbele cha msingi na cha kuamua.
“Kwa bahati mbaya, maombi ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamefanikiwa kwa asilimia 37 au 38 tu,” alisema kwa masikitiko, akiapa kuendelea na juhudi za kutetea msaada kwa watu walioko katika hali ngumu.
Mchakato wa amani kwa RDC ulikuwa kiini cha mazungumzo kati ya Thérèse Wamba na Jean-Pierre Lacroix.
Lacroix aliwasili Kinshasa Jumapili usiku kwa ziara rasmi ya siku tano. Ratiba yake inajumuisha mazungumzo na viongozi, upinzani, na asasi za kiraia za Kongo kuhusu mchakato wa amani nchini RDC.
Leonard Sangwa